Habari za kuaminika kutoka maeneo ya pwani na kaskazini mashariki mwa Kenya

Friday, 21 November 2014

SUPKEM YATAKA WASIMAMIZI WA USALAMA MOMBASA WAONDOLEWE

Viongozi wa baraza kuu la Waislamu nchini Kenya, (Supkem) kutoka kaunti ya Garissa wametoa wito kwa serikali itekeleze mabadiliko kwa wasimamizi wa uslama mjini Mombasa kwa kutowajibika.

Wakizungumza mjini Garissa mapema leo, viongozi hao wakiongozi na Mwenyekiti wa Supkem mjini humo, Abdullahi Salat, wamewalaumu maafisa wakuu wa uslama mjini Mombasa kwa ongezeko la visa vya utovu wa usalama.

"Tunamuomba Rais Uhuru Kenyatta, awafanyie mabadiliko Wakuu wa usalama mjini Mombasa, kwa sababu wengi wao wamekuwa na ukatili dhidi ya wenyeji wanaostahili kuwalinda na hivyo basi kusababisha kutoaminiana", Abdullahi amesema.

Aidha viongozi hao wamelaani vikali hatua ya kufungwa kwa misikiti na kufurushwa kwa waumini mara kwa mara huku wakidai kuwa huenda hali hiyo ikaathiri uwiano mjini humo. Badala yake, viongozi hao wameiri serikali kutumia mbinu mbadala za kupambana na washukiwa wa uhalifu bila kuwalenga waumini.

Vilevile, Abdullahi amewaonya maafisa wa usalama dhidi ya kulenga misikiti huku akieleza kuwa misikiti ni eneo muhimu la ibada wala sio maskani ya wahalifu.

Viongozi hao wa Supkem wameongeza kuwa viongoi wa kidini ndio wanaostahili kulifumbua tatizo linalosibu mjini Mombasa kwa njia ya mazungumzo wala sio kupitia maafisa wa usalama.

Haya yanajiri baada ya maafisa kutoka vikosi mbalimbali vya usalama kuvamia misikiti ya Musa, Sakina na Swafaa na kuwakamata zaidi ya vijana 200.


Kwa sasa, Misikiti hiyo iko chini ya ulinzi mkali huku wenyeji wakilazimika kusaka njia mbadala za kutekeleza Ibada.

No comments:

Post a Comment