Habari za kuaminika kutoka maeneo ya pwani na kaskazini mashariki mwa Kenya

Thursday, 31 July 2014

Mkufunzi wa Bandari, Twahir Muhiddin alazwa hospitalini

Kocha wa Bandari, Twahir Muhiddin
Kocha Twahir Muhiddin anayewafunza wawakilishi wa pwani katika ligi kuu ya soka humu nchini, Bandari, anaendelea kupokea matibabu katika hospitali moja mjini Mombasa baada ya kuugua.

Akithibitisha taarifa hiyo, meneja wa bandari, Charles Obwaka ameeleza kuwa Twahir amelazwa hospitalini siku ya jumamosi baada ya kupatwa na maumivu.

Obwaka ameongeza kuwa wanamatumaini kuwa Twahir atarejea katika hali ya kawaida na kuendelea kuinoa timu hiyo inayoshikilia nafasi ya kumi na moja kwenye jedwali la ligi kuu ya soka humu nchini.

Kutokuwepo kwa Twahir haikuathiri timu hiyo kwani Bandari ilijitahidi na kuondoka na sare ya goli moja dhidi ya Tusker kwenye mchuano wa ligi ulioandaliwa katika uwanja wa Mombasa siku ya jumapili.

Kufikia sasa manaibu wakufunzi wa Bandari, Ali Breik na Nassoro Mwakoba wanaendelea kuifunza timu hiyo kwa minajili ya mchuano wake wa ligi ugenini dhidi ya Mathare itakayochezwa tarehe sita mwezi ujao.

Gavana Joho amtimua waziri wa fedha, Walid Khalid

Aliyekuwa waziri wa fedha, kaunti ya Mombasa, Walid Khalid
Baada ya vuta nikuvute kati ya bunge la kaunti ya Mombasa na waziri wa Fedha, Walid Khalid, hatimaye Gavana wa Mombasa Hassan Ali Joho amemuachisha kazi waziri wake wa fedha, Walid Khalid.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Joho amekariri kuwa amechukua hatua hiyo baada ya misururu ya Khalid kukumba na madai ya ukiukaji wa sheria za utoaji zabuni na ununuzi wa mahitaji ya serikali ya  kauti ya Mombasa.

Awali wabunge wa kaunti ya Mombasa waliwasilisha hoja ya kutokuwa imani na Khalid huku wakidai kuwa hawajapendezwa na utendakazi wake.

Kwa sasa Gavana Joho amemteua waziri wa vijana na michezo, Hazel Koitaba kuwa kaimu waziri wa fedha huku gavana huyo akisubiriwa kumteuwa waziri mpya wa fedha.



Uanzilishi wa taa za trafiki Mombasa, zapongezwa

Taa za trafiki zikimulika barabarani

Wamiliki wa magari ya uchukuzi mjini Mombasa wameipongea serikali ya kaunti ya Mombasa kwa kufanikisha taa za trafiki.

Wakiongozwa na mfanyibiashara maalum,na mmiliki wa kampuni moja ya mabasi, Mohamed Ibrahim, wafanyibiashra hao wameeleza kuwa taa hizo zimepunguza ajali za barabara pamoja na msongamano wa magari mjini Mombasa.

Kwa upande wake waziri wa uchukuzi mjini Mombasa, Mohamed Abbass, ametoa ufafanuzi kuwa serikali ya kaunti hiyo imechukua hatua hiyo kama njia moja ya kuimarisha sekta ya uchukuzi mjini humo.

Abbass ameongeza kuwa serikali hiyo inalenga kuzidisha idadi ya taa hizo katika maeneo mengine mjini humo ili kuzuia msongamano wa magari na ukiukaji wa sheria za barabarani.

Taa hizio zimewekwa katika barabara mbalimbali kama vile, Buxton, Digo na Sabasaba.





Viongozi wa Mombasa wataka miraa ipigwe marufuku

Zao la miraa linalotaka kupigwa marufuku
Viongozi mbalimbali mjini Mombasa, wameapa kuhakikisha kuwa zao la miraa limepigwa marufuku mjini humo huku wakiilaumu kwa uzembe na kudorora kwa afya ya wakazi wa mji huo.

Wakiongozwa na mbunge wa Changamwe, Omar Mwinyi na mwenzake wa Jomvu, Badi Twalib, na wabunge mbalimbali wa kaunti, viongozi hao wamemrai gavana wa mombasa, Hassan Ali Joho, apige marufuku uuzaji na utumizi wa miraa huku viongozi hao wakidai kuwa idadi kubwa ya wenyeji wa kaunti hiyo wameathirika pakubwa na matumizi ya zao hilo huku mamilioni ya fedha zikitumika kwa ununuzi wake.

Kwa upande wao wabunge wa kaunti wametoa wito kwa wabunge wenzao waunge mkono mpango huo huku wakihoji kuwa hatua hiyo itakuw ana manufaa makubwa kwa maendeleo ya kaunti hiyo.

Kauli ya viongozi hawa inajiri wiki chache tu baada ya bunge la kaunti ya Mombasa kupinga mswada dhid ya miraa uliowasilishwa na mwakilishi wa wodi mteule, Fatma Swaleh.

Madereva wengi mjini Mombasa wamelaumiwa kwa kuendesha magari wakitumia miraa huku wakihatarisha maisha ya maabiria.

Hata hivyo mamlaka ya kitaifa ya kudhibiti vileo na mihadarati, Nacada, imeambia serikali ya kaunti ya mombasa iuende sheria itakayoongoza juu ya uuzaji na utumiaji wa miraa katika maeneo muhimu mjini humo.

Mtalii wa Kijerumani auwawa Mombasa

Watalii wakiwasili humu nchini
Taharuki imetanda mjini Mombasa baada ya mtalii mmoja kutoka Ujerumani kuuwawa kwa kupiga risasi katika mtaa wa Mji wa Kale, mjini Mombasa usiku wa kuamkia leo.

Mtalii huyo, ChristineTex mwenye umri wa miaka 30, alifariki papo hapo baada ya watu waliojihami kwa bnduki kuwamiminia risasi yeye pamoja na mchumba wake, Henri Sekandi.

Kulinga na mkuu wa idara ya polisi wa utalii, mjini Mombasa,Robert Sicharani, mwanamke huyo alikuwa pamoja na mchumba wake kutoka Uganda huku wawili hao wakiwa katika ziara ya kitalii katika mji wa kihistoria wa Mji wa kale.

Kwa upande wake, Khalid Ibrahim, ambaye ni msimamizi wa polisi jamii katika mtaa wa mji wa kale, ameeleza kuwa mwanamke huyo aliuwawa bila kuibiwa chochote huku kiini cha mauaji yake kikisalia kuwa kitendawili.

Mji wa Kale umekuwa ukishuhudia mauaji ya watalii ya mara kwa mara kwani miezi michache iliyopita, watalii watatu kutoka urusi walishambuliwa na kuuwawa kwa kupigwa risasi.

Polisi wanaendeleza uchunguzi ili kubaini chanzo cha mauaji hayo.

Sunday, 6 July 2014

Zaidi ya watu 30 wauwawa katika kaunti za Lamu na Tana River

Wakaazi wakisaidiana na mfanyikazi wa Red Cross kumhudumia mhasiriwa















Hofu na huzuni zimetanda katika maeneo ya Gamba, Kaunti ya Tana river na Hindi, Kaunti ya Lamu baada ya zaidi ya watu 30 kuuwawa kwa kupigwa risasi kwenye Mashambulizi mawili yaliyotekelezwa usiku wa kuamkia leo.

Kulingana na kamanda wa polisi katika kanda ya Pwani, Robert Kitur, watu 9 akiwemo afisa mmoja wa polisi wameuwawa huku mtu mmoja akijeruhiwa vibaya katika eneo la Gamba, mji wa Garseni baada ya watu waliojihami kwa risasi kukivamia kituo cha polisi cha Gamba  na kumtorosha mshukiwa mmoja wa mauaji ya mpeketoni aliyekuwa anazuiliwa kwenye kituo hicho.

Wakati huo huo watu saba wameuwawa katika eneo la Hindi,lililoko kilomita chache kutoka mji wa Mpeketoni ambapo zaidi ya watu 60 waliuwawa katika hali ya kutatanisha majuma kadhaa yaliyopita.

Kwenye tukio la Hindi, nyumba kadhaa na magari ya meteketezwa huku watu watano walio na majeraha mabaya ya risasi wakiendelea kuuguza majeraha katika hospitali ya King Fahad, kaunti ya Lamu.

Kituo cha kitaifa cha kukabiliana na majanga, NDOC kimesimulia kupitia ukurasa wake wa twitter kuwa makabiliano makali ya risasi yalizuka katika eneo la kibiashara la Hindi karibu na Mpeketoni, usiku wa kuamkia leo.

Maafisa wa polisi wakishirikiana na shirika la red cross wanaendelea na operesheni ya kuwaokoa wahasiriwa huku wakiwasaka wavamizi hao.

Hata hivyo kiini cha mauaji hayo hakijabainika huku msemaji wa kundi la wanamgambo wa Al shabab, Abdulazizi Abu Musab akikiri kuwa kundi hilo limetekeleza ukatili huo jambo ambalo Rais Uhuru Kenyatta amelpinga vikali na kuhoji kuwa mauji hayo yamechochewa kisiasa.

Uvamizi huu unajiri licha ya serikali kuwahakikishia raia usalama wao huku mrengo wa upinzani wa Cord ukitarajiwa kuandaa mkutano wake wa Sabasaba katika bustani la Uhuru, jijini Nairobi, hapo kesho. 

Thursday, 3 July 2014

Mwezi wa Ramadhan yawanufaisha wanabiashara Mombasa

Muuzaji akiwa na mteja kwenye kibanda cha kuuza vyakula

















Wafanyibiashara wa Mombasa wanaendelea kufurahia mapato ya uuzaji wa bidhaa mbalimbali kwenye mwezi wa ramadhan huku waumini wa kiislamu wakitekeleza ibada ya saum.

Wafanyibiashara wa soko la Markiti, mwembe tayari na soko kuu la kongowea wameshuhudia ongezeko la wateja huku biashara zao zikipigwa jeki na hatua ya serikali ya kaunti ya Mombasa ya kuondoa marufuku kwa wachuuzi wa vyakula katika maeneo ya kibiashara mjini humo.

Wengi wa Wafanyibiashara wanaoendelea kunufaika ni wauzaji wa vyakula na vifaa vya nyumbani huku ongezeko la bei za bidhaa hizo likishuhudiwa kutokana na maandalizi ya mlo wa kufungua saumu jioni wa iftar na mlo wa mwisho wa usiku wa daku na waumini wa kiislamu.

Tende, madafu, unga, matunda, mboga na nyama ni baadhi ya bidhaa zenye mvuto mkubwa kwa wateja hao kutokana na umuhimu wa bidhaa hizo katika mwezi wa Ramadhan.

Waumini hao wa kiislamu hutekeleza ibada ya saum ya siku 29 au 30 kila mwezi wa tisa katika kalenda ya kiislamu.