Habari za kuaminika kutoka maeneo ya pwani na kaskazini mashariki mwa Kenya

Thursday, 26 June 2014

Hatujarudisha hata senti kwa serikali kuu,asema Gavana wa Garissa, Nathif Jama

Ismail Haki, kutoka shirika la TIKA (kulia) na Gavana wa Garissa, Narthif Jama.















Gavana wa Kaunti ya Garissa, Nathif Jama, amepuuzilia mbali madai kuwa serikali yake imerudisha bilioni moja nukta mbili ya pesa iliyotengewa na serikali kuu kwa minajili ya maendeleo ya kaunti hiyo.
 
Akiwahutubia wananchi katika mji wa Garissa baada ya kupokea magari ya kuokota taka yaliyotolewa na shirika la kituruki la TIKA, Jama alijitetea na kusema kuwa waliutumia mgao wao vyema "Kaunti yetu haiwezi ikachukua hatua kama hiyo . Tumezitumia fedha tulizotengewa kufadhili miradi mbalimbali katika kaunti hii", alisema.

Nathif ametofautiana na ripoti hiyo iliyowasilishwa kwa bunge la seneti na msimamizi wa bajeti huku akihoji kuwa serikali yake imeshuhudia upungufu wa fedha kinyume cha madai kuwa haikuweza kutumia fedha ilizotengewa vikamilifu.

Wakati huo huo, Gavana huyo ameishukuru serikali ya uturuki kwa msaada huo huku akiwataka wenyeji wa mji huo kuyatumia magari hayo vyema ili kufanikisha usafi katika mji huo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa serikali ya Uturuki, Ismail Haki, ameahidi kuwa serikali hiyo itaendelea kuunga mkono miradi ya maendeleo katika kaunti hiyo na serikali ya Kenya.

"Tutaendelea kufanya kazi na wenyeji wa kaunti ya Garissa ili kuboresha maisha yao. Tulikuwa pamoja wakati wa kiangazi na tutazidi kushirikiana nanyi," alimaliza bwana Ismail.

Msaada huo wa magari umepiga jeki hatua za kuleta usafi katika mji huo huku wenyeji wakijawa na matumaini kuwa magari hayo yatatumika vyema.

Arsenal yawatimua wachezaji kumi na moja


Miamba wa soka nchini uingereza na mabingwa wa Kombe la F.A, Arsenal fc imetangaza rasmi kuwa imetengana na wachezaji kumi na moja wa timu hiyo ili kutoa nafasi kwa wachezaji wanaotaka kuwasajili.

Kupitia taarifa kwenye mtandao wake wa Arsenal.com, mshambulizi matata wa Denmark, Niklas Bendtner na nahodha wa zamani wa Korea kusini J.Y Park wameihama timu hiyo baada ya mkataba wao kumalizika.

Wakati huo huo, wachezaji waliojiunga na timu hiyo kwa njia ya mkopo, Kim Kallstrom wa Sweden na kipa Emiliano Viviano watarejea kwa wamiliki wao baada ya kutumikia mda wao wa mkopo ugani emirates.

Aidha mdakaji Lukasz Fabianski, beki Bacary Sagna na kiungo Zak Ansah wameihama timu hiyo baada ya kudinda kurefusha kandarasi zao an timu hiyo.

Wengine walioigura timu hiyo ni wachezaji chipukizi, Chuks Aneke na Daniel Boateng, Zach Fagan na Leander Siemann.

Kutoka hapa mtitigo, tunawatakia mastaa hao kila la heri popote watakapokwenda kusakata kambumbu.





Chuo kikuu cha Technical University of Mombasa chafungwa






















Shughuli za masomo zimekatizwa katika tawi kuu la chuo kikuu cha kiufundi cha Mombasa  kufuatia mgomo wa wanafunzi wa chuo hicho.

Wanafunzi wa kozi za uhandisi wanadaiwa kuanzisha mgomo huo huku wakidai kuwa chuo hicho hakina uwezo wa kutoa kozi hiyo na badala yake sasa wanataka wahitimu kozi hiyo katika chuo kikuu cha kilimo na teknolojia Jomo kenyatta.

Hata hivyo wanafunzi hao hawajasababisha uharibifo wowote licha ya maafisa wa polisi kuingilia kati na kuufurusha mgomo huo kwa kutumia vitoa machozi.

Kwa sasa wasimamizi wa chuo hicho wanaendelea na mazungumzo kwenye mkutano wa dharura ili kulifumbua tatizo hilo.

Wanafunzi wote wa chuo hicho wamepewa ilani ya kuondoka haraka iwezekananvyo hadi pale watakapofahamishwa tarehe mpya ya kufunguliwa kwa chuo hicho.


Wednesday, 25 June 2014

Gavana wa Lamu, Issa Timamy matatani kwa mauaji ya Mpeketoni

Gavana wa Kaunti ya Lamu, Issa Timamy.
Gavana wa kaunti ya Lamu Issa Timamy anatarajiwa kufikishwa mahakamani hii leo kufuatia mauaji ya hivi majuzi ya zaidi ya watu 60 katika eneo la Mpeketoni, kaunti ya Lamu.

Gavana Timamy alikamatwa mjini Mombasa siku ya Jumatano na maafisa wa idara ya upelelezi ya CID na kuzuiliwa katika afisi za idara hiyo kwa saa kadhaa ili kuhojiwa.

Kaunti ya Lamu imekuwa chini ya kurunzi kali ya serikali kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara yaliyotekelezwa na watu wasiojulikana na kuwa tishio kubwa kwa usalama wa wenyeji wa kaunti hiyo.

Hata hivyo chanzo cha mauaji katika kaunti hiyo hakijabainika kufikia sasa licha ya Rais Uhuru Kenyatta kueleza kuwa uvamizi katika eneo la mpeketoni lilichochewa kisiasa.

Kundi la wanamgambo la Al Shabaab lilijitokeza na kukiri kuwa lilitekeleza shambulizi la eneo la Mpeketoni huku kundi hilo likiitaka serikali iwaondoe wanajeshi wake walioko nchini Somalia.

Timamy aliponea na kusalia kuwa gavana mnamo mwezi Novemba mwaka uliopita baada ya mahakama ya rufaa kufutilia mbali uchaguzi mdogo wa ugavana ulioratibiwa kufanywa na tume huru ya uchaguzi na mipaka, IEBC.

Monday, 23 June 2014

Watu 30 wauwawa katika kaunti za Wajir na Mandera



Viongozi wa Kaunti za Wajir na Mandera wakiwa katika eneo la Wajir

















Huzuni imetanda katika kaunti za Wajir na Mandera baada ya watu 30 kufariki kufuatia mapigano mapya kati ya jamii za Garre na Degodia.

Akithibitisha mauaji hayo, Msemaji wa polisi Gatiria Mboroki amesema kuwa watu wa koo ya Gegodia wanadai wizi wa mifugo yao na mahasimu wao kutoka jamii ya Gare na kupelekea vita hivyo katika eneo la Gunan.

Wakati huo huo, familia 35 zimeachwa bila makao baada ya nyumba zao kuteketezwa kwenye mapigano hayo huku watu watano wakijeruhiwa vibaya.

Maafisa kutoka kitengo cha GSU, polisi wa kawaida na KDF wa kambi ya Elwak wametumwa eneo hilo kudhibiti hali huku kukiwa na ripoti kwamba watu wengine watano walijeruhiwa vibaya kwenye ghasia hizo na nyumba 35 kuteketezwa.

Kiongozi wa waliowengi bungeni, Aden Dualle amelaani vikali mauaji hayo huku akiongeza kuwa jamii hizo zinastahili kukumbatiua amani ili kuzuia umwagikaji wa damu.

Mradi wa ujenzi wa barabara ulioanzishwa na serikali ya kaunti ya Wajir umelaumiwa kwa mapigano hayo huku jamii hizo zikiendelea kuzozania mpaka kati ya kaunti hizo.
Hatua za viongozi wa kisiasa na wa kidini kuzipatanisha koo hizo mbili zimegonga mwamba huku hali ya taharuki ikitanda kati ya watu wa jamii hizo mbili.

Kwa sasa wenyeji wa kaunti hizo wanaitaka serikali iwakamate viongozi wa kisiasa kwa uchochezi  huku watu 40 wakiwa wamefariki na wengine wafikao 100 wakiachwa bila makao ndani ya kipindi cha  mwezi moja tu kwenye ghasia hizo.