Habari za kuaminika kutoka maeneo ya pwani na kaskazini mashariki mwa Kenya

Monday, 23 June 2014

Watu 30 wauwawa katika kaunti za Wajir na Mandera



Viongozi wa Kaunti za Wajir na Mandera wakiwa katika eneo la Wajir

















Huzuni imetanda katika kaunti za Wajir na Mandera baada ya watu 30 kufariki kufuatia mapigano mapya kati ya jamii za Garre na Degodia.

Akithibitisha mauaji hayo, Msemaji wa polisi Gatiria Mboroki amesema kuwa watu wa koo ya Gegodia wanadai wizi wa mifugo yao na mahasimu wao kutoka jamii ya Gare na kupelekea vita hivyo katika eneo la Gunan.

Wakati huo huo, familia 35 zimeachwa bila makao baada ya nyumba zao kuteketezwa kwenye mapigano hayo huku watu watano wakijeruhiwa vibaya.

Maafisa kutoka kitengo cha GSU, polisi wa kawaida na KDF wa kambi ya Elwak wametumwa eneo hilo kudhibiti hali huku kukiwa na ripoti kwamba watu wengine watano walijeruhiwa vibaya kwenye ghasia hizo na nyumba 35 kuteketezwa.

Kiongozi wa waliowengi bungeni, Aden Dualle amelaani vikali mauaji hayo huku akiongeza kuwa jamii hizo zinastahili kukumbatiua amani ili kuzuia umwagikaji wa damu.

Mradi wa ujenzi wa barabara ulioanzishwa na serikali ya kaunti ya Wajir umelaumiwa kwa mapigano hayo huku jamii hizo zikiendelea kuzozania mpaka kati ya kaunti hizo.
Hatua za viongozi wa kisiasa na wa kidini kuzipatanisha koo hizo mbili zimegonga mwamba huku hali ya taharuki ikitanda kati ya watu wa jamii hizo mbili.

Kwa sasa wenyeji wa kaunti hizo wanaitaka serikali iwakamate viongozi wa kisiasa kwa uchochezi  huku watu 40 wakiwa wamefariki na wengine wafikao 100 wakiachwa bila makao ndani ya kipindi cha  mwezi moja tu kwenye ghasia hizo.

No comments:

Post a Comment